Msaada · WhatsApp

Kuunganisha namba yako mwenyewe ya WhatsApp

Jinsi ya kufungua WhatsApp Business API kwa Meta, na kuiunganisha na SUHU — namba ikibaki yako, bili ya Meta ikiwa yako, na mazungumzo yote yakiingia kwenye inbox yako ya SUHU.

Njia mbili

Kuna njia mbili za kupata namba inayofanya kazi na SUHU. Chagua kabla hujaanza, kwa sababu zinatofautiana sana kwa muda na kwa kazi.

1. Tunakufanyia (rahisi)

Unaingia SUHU → SettingsChannels → “Get your own WhatsApp number”, unatuambia namba na jina la biashara, sisi tunashughulika na Meta. Hii inafaa kama huna akaunti ya Meta Business wala huna muda wa kupitia mchakato wote.

2. Unajifanyia (ukurasa huu)

Unafungua akaunti yako ya Meta Business, unasajili namba yako mwenyewe, unatengeneza token yako — kisha unatupa thamani tatu tu. Faida: bili ya Meta inaenda kwako moja kwa moja, na namba pamoja na akaunti ya WhatsApp Business ni mali yako kabisa.

Kabla hujaanza

Vitu vinne. Ukikosa kimoja, mchakato unakwama katikati:

  • Namba ya simu isiyokuwa kwenye WhatsApp. Hii ndiyo inayowakwamisha watu wengi. Kama namba ipo kwenye WhatsApp au WhatsApp Business app, lazima ufute akaunti hiyo kwanza (WhatsApp → Settings → Account → Delete my account) au utumie laini nyingine kabisa. Namba ya ofisi isiyotumika kwenye simu inafaa zaidi.
  • Akaunti ya Facebook unayoweza kuingia nayo.
  • Vielelezo vya biashara — jina rasmi, anwani, na kitu kinachothibitisha biashara ipo (leseni ya biashara, TIN, au bili ya huduma yenye jina la biashara). Meta inaomba hivi wakati wa business verification.
  • Tovuti au ukurasa wa Facebook wa biashara. Meta inauliza.
Muda Kufungua na kutuma ujumbe wa kwanza kunaweza kuchukua saa chache. Lakini business verification ya Meta inaweza kuchukua siku kadhaa hadi wiki, na huwezi kuiharakisha. Anza mapema kama una tarehe unayoilenga.

Hatua za upande wa Meta

Meta hubadilisha majina ya vitufe na mpangilio wa kurasa mara kwa mara. Hapa nimeeleza kitu cha kutafuta badala ya njia kamili ya kubofya, na kwa sehemu zinazobadilika mara nyingi, nimeweka kiungo cha nyaraka zao rasmi.

  1. Fungua Meta Business Account

    Nenda business.facebook.com, tengeneza akaunti ya biashara kwa jina rasmi la biashara yako (siyo jina lako binafsi). Hii ndiyo itakuwa mwavuli wa kila kitu kingine.

  2. Anza business verification mara moja

    Ndani ya Business Settings, tafuta Security Centre au Business verification na anza mchakato. Ndiyo sehemu inayochukua muda mrefu kuliko zote, kwa hiyo ianze siku ya kwanza, siyo baada ya kumaliza mengine.

    Bila verification utaweza kujaribu, lakini utakuwa na kikomo kidogo cha watu unaoweza kuwatumia ujumbe kwa siku.

  3. Tengeneza app kwenye Meta for Developers

    Nenda developers.facebook.com/appsCreate App. Chagua aina inayohusiana na biashara/“Other”, kisha ongeza product ya WhatsApp kwenye app hiyo. Iunganishe na Business Account uliyoifungua hatua ya kwanza.

  4. Ongeza namba yako

    Ndani ya WhatsApp → API Setup (au “Getting started”), ongeza namba yako halisi ya biashara na uthibitishe kwa SMS au simu. Hapa pia unaweka display name — jina litakaloonekana kwa wateja. Meta inalikagua; jina linalodanganya au lisilolingana na biashara linakataliwa.

  5. Tengeneza token ya kudumu

    Token unayoiona kwenye ukurasa wa API Setup ni ya saa 24 tu — haifai kwa mfumo unaofanya kazi kila siku. Unachohitaji ni System User token:

    • Business Settings → UsersSystem Users → tengeneza mmoja (aina: Admin au Employee).
    • Mpe ruhusa (Assign assets) juu ya WhatsApp Business Account yako na app yako.
    • Bofya Generate new token, chagua app yako, kisha chagua ruhusa whatsapp_business_messaging na whatsapp_business_management.
    • Chagua muda: Never expire kama chaguo hilo lipo.

    Nakili token hiyo mara moja — haitaonekana tena.

Nyaraka rasmi za Meta Hatua za kina zaidi na picha zipo hapa: WhatsApp Cloud API — Get Started. Zikitofautiana na ukurasa huu, ukweli uko upande wao — na tuambie ili tuurekebishe.

Thamani tatu unazohitaji

Baada ya hatua za juu, unakuwa na vitu vitatu tu vya kutuletea:

KituUnakipata wapiKinaonekanaje
Phone number ID WhatsApp → API Setup, chini ya namba yako 123456789012345
WhatsApp Business Account ID Ukurasa uleule wa API Setup (WABA ID) 987654321098765
Access token System User uliyoitengeneza hatua ya 5 EAAG… (herufi ndefu sana)
Usichanganye hizi mbili Phone number ID na WABA ID zinafanana kabisa — namba ndefu za tarakimu 15. Zikibadilishana, kutuma kunashindwa kila mara na ujumbe wa hitilafu hauelezi kwa nini. Nakili kila moja kutoka mahali pake, siyo kwa kukumbuka.
Token ni kama nenosiri Mtu mwenye token yako anaweza kutuma ujumbe kwa jina la biashara yako. Usiituma kwa WhatsApp wala barua pepe ya kawaida. Iweke wewe mwenyewe kwenye SUHU — inahifadhiwa ikiwa encrypted, na haionyeshwi tena baada ya kuihifadhi.

Kuziweka kwenye SUHU

Thamani hizi haziwekwi na wewe mwenyewe — zinawekwa na timu ya SUHU. Siyo urasimu: namba iliyoandikwa vibaya kwa tarakimu moja inashindwa kutuma kila mara bila kueleza kwa nini, na hiyo ni siku ya kupoteza kwa mtu asiyejua atazamie wapi. Tunaziweka, tunajaribu, kisha tunakuthibitishia.

  1. Ingia SUHU → Settings → kichupo cha Channels.
  2. Kwenye fomu ya “Get your own WhatsApp number”, jaza namba, jina la kuonekana, na — kwa kuwa tayari unazo — Phone number ID na WhatsApp Business Account ID.
  3. Weka access token yako kwenye sehemu yake ya siri iliyo chini ya hizo. Usiiandike kwenye sehemu ya maelezo.
  4. Kwenye sehemu ya maelezo, andika kwamba tayari umefungua app yako mwenyewe Meta, ili tusianze upya.
  5. Tuma.
Token yako inashughulikiwaje Inahifadhiwa ikiwa encrypted mara tu unapotuma, na hairudi kuonyeshwa kwa mtu yeyote — wala kwako, wala kwetu. Inatumika mara moja kuunganisha workspace yako, kisha inafutwa kwenye ombi. Ndiyo maana ina sehemu yake badala ya kuandikwa kwenye maelezo.
Ukiamua kutotoa token yako Bila token yako mwenyewe, SUHU inatumia token ya platform. Kila kitu kinafanya kazi — lakini ujumbe unalipiwa kwenye akaunti ya Netpoa, siyo yako. Ukitaka bili ya Meta iwe yako moja kwa moja, token yako inahitajika.

Baada ya kuunganishwa, jaribu mara moja: mwambie mtu akutumie ujumbe kwenye namba hiyo. Ukiuona kwenye inbox ndani ya sekunde chache, umemaliza.

Webhook na app secret

Soma hii kabla hujajaribu kuweka webhook mwenyewe Usiweke webhook ya app yako mwenyewe ielekee SUHU. Haitafanya kazi, na utapoteza siku mbili ukijaribu kujua kwa nini.

SUHU ina endpoint moja ya webhook kwa mfumo mzima (https://suhu.co.tz/webhooks/whatsapp), na inathibitisha sahihi ya kila ujumbe unaoingia kwa app secret moja ya platform. App yako mwenyewe ingekuwa na app secret yake tofauti — kwa hiyo kila ujumbe kutoka kwake ungekataliwa kimya kimya kama ujumbe bandia.

Kwa hiyo mgawanyo halisi ni huu:

KituNi cha nani
Namba ya simuYako
WhatsApp Business Account (WABA)Yako
Access token na bili ya MetaYako
TemplatesZako
App inayopokea webhookYa SUHU

Ili WABA yako ipeleke mazungumzo kwenye SUHU, inaunganishwa na app ya SUHU — hatua tunayoifanya sisi upande wetu baada ya kupokea thamani zako tatu. Hii ndiyo njia ya kawaida ya watoa huduma wote wa WhatsApp (Business Solution Providers), siyo kitu cha kipekee cha SUHU.

Unahitaji app yako kabisa, ikiwa na app secret yako, ikituma webhook moja kwa moja kwa SUHU? Haiwezekani leo, lakini tuambie kwa nini unaihitaji — kama biashara kadhaa zinaihitaji, tunaweza kuijenga.

Templates na sheria ya saa 24

Hii siyo sheria ya SUHU — ni ya Meta, na inatumika kwa kila mtu:

  • Mteja akikutumia ujumbe, unafunguka dirisha la saa 24. Ndani yake unaweza kumjibu maandishi ya kawaida, chochote unachotaka.
  • Nje ya saa 24, huwezi kuandika ujumbe wa kawaida. Lazima utumie template iliyoidhinishwa na Meta.

Templates zinatengenezwa upande wa Meta: Business Settings → WhatsApp ManagerMessage TemplatesCreate template. Uidhinishaji huchukua kutoka dakika chache hadi saa kadhaa.

Zinazokataliwa mara nyingi ni zile zinazoonekana kama matangazo kwa mtu asiyekubali, au zenye maneno ya kubahatisha. Template ya kumbusho la malipo, uthibitisho wa oda, au taarifa ya huduma hupita kwa urahisi.

SUHU inasoma templates zako yenyewe Ukiweka WABA ID yako, SUHU inasoma orodha ya templates zilizoidhinishwa moja kwa moja kutoka Meta — huhitaji kuziandika tena hapa.

Matatizo ya kawaida

“Ujumbe unashindwa kutumwa, hakuna sababu iliyo wazi”

Mara nyingi ni phone number ID iliyowekwa mahali pa WABA ID au kinyume chake. Ziangalie tena kwenye API Setup. Kama wewe ni mteja wa SUHU, tunaona sababu halisi ya Meta kwenye ukurasa wa logs — tuulize.

“Session has expired”

Umetumia token ya saa 24 ya ukurasa wa API Setup badala ya System User token. Rudi hatua ya 5.

“Namba yangu inakataliwa”

Bado ipo kwenye WhatsApp au WhatsApp Business app. Futa akaunti hiyo kutoka kwenye simu kwanza, kisha subiri dakika kadhaa ujaribu tena.

“Ujumbe unaingia lakini majibu hayafiki”

Mara nyingi ni dirisha la saa 24 limefungwa. Angalia mazungumzo yalipoanza — kama ni zaidi ya saa 24, unahitaji template.

“Kila kitu kipo sawa lakini hakuna kinachoingia”

WABA yako pengine bado haijaunganishwa na app ya SUHU. Hilo ni jambo la upande wetu — tutumie barua pepe na tuangalie.

Umekwama mahali?

Tuambie ulipofikia na ujumbe wa hitilafu ulioupata. Mara nyingi ni thamani moja iliyobadilishana.

Tuandikie