Mteja anachagua saa kwenye ukurasa wako, analipia kabla, kisha anakupigia WhatsApp kwa saa hiyo. Muda unahesabiwa wenyewe, na ukiisha simu inakatika. Hakuna kudai, hakuna kusahau, hakuna simu ya saa mbili iliyolipiwa moja.
Mteja hahitaji app wala akaunti. Anapiga WhatsApp kama anavyopiga mtu yeyote.
Miadi inapangwa kwa ujumbe, malipo yanafuatiliwa kwa kumbukumbu, na simu inaenda muda wowote. Kila kipande kiko mahali pake, na hakuna kinachoongea na kingine.
Ulikubali na wawili kwa WhatsApp, siku tofauti, na umegundua asubuhi ya siku yenyewe. Mmoja anarudishwa, na hatarudi.
Huwezi kumkatiza mtu anayeeleza tatizo lake. Kwa hiyo unaendelea, na miadi inayofuata inachelewa, na siku yako inavunjika.
Umeshatoa ulichokuwa nacho. Kudai baada ya hapo ni mazungumzo magumu kuliko ushauri wenyewe, na wengine hawalipi kabisa.
Jumatatu hadi Ijumaa, 09:00 hadi 13:00. Mapumziko ni kipande cha pili. Unaamua nafasi moja ni dakika ngapi.
Mteja anachagua saa iliyo wazi na anaacha namba yake. Nafasi moja haiwezi kuchukuliwa na watu wawili.
Ukishathibitisha malipo, dakika zinawekwa kwenye namba yake. Bila malipo, hakuna simu.
Simu inaita kwenye SUHU yako. Unaona muda ukipungua, na ukiisha simu inakatika yenyewe.
Link yako mwenyewe, inayoonyesha saa zako zilizo wazi pekee. Mteja anachagua, anaacha namba, na ndiyo hiyo.
Saa inaonekana mbele yako ukiwa kwenye simu. Dakika mbili za mwisho zinakuwa nyekundu, dakika moja inasikika, kisha inakatika.
Ujumbe wote wa wateja mahali pamoja, siyo kwenye simu yako binafsi. Msaidizi wako anaweza kuingia bila kupewa simu yako.
Inajibu maswali ya kawaida, inaeleza bei na jinsi ya kujiunga, na inakuachia muhtasari wa kila simu iliyoingia.
Nani alipiga, lini, kwa muda gani, na nini kilizungumzwa. Mteja akirudi mwezi ujao, unajua mlipoishia.
Dakika zilizouzwa, zilizotumika, zilizobaki na mapato — hesabu zinazolingana na zilizopo kwenye akaunti yako.
Kinachofanya kazi sasa: ukurasa wa kujiunga na saa zako, kuzuia nafasi moja kuchukuliwa mara mbili, kuweka dakika kwa namba ya mteja, simu ya WhatsApp na saa inayoikata muda ukiisha, inbox, AI, kumbukumbu za simu na hesabu za fedha.
Bado hakipo: vikumbusho vya kiotomatiki kabla ya miadi. Kwa sasa unamkumbusha mteja mwenyewe kwa WhatsApp.
Malipo: mteja analipa kwa M-Pesa au Tigo Pesa kwako moja kwa moja, kisha wewe unathibitisha kwenye SUHU na dakika zinawekwa mara moja. Malipo ya kiotomatiki yanakuja.
Hauhitaji wateja wapya. Wale unaowahudumia sasa kwa WhatsApp ndio wa kuanza nao — tofauti ni kwamba wanajua saa, wanalipa kabla, na siku yako haivunjiki tena.